Description
Kitabu cha Mwongozo wa Uandishi wa Insha
Kitabu hiki kinamwelekeza mwanafunzi katika uandishi wa insha mbalimbali. Wanafunzi wengi pamoja na walimu hukwepa kipengele cha insha kwa madai kuwa hakivutii; jambo ambalo linasababisha matokeo mabaya. Kutokana na haya, kitabu hiki kinatoa maelekezo kwa wanafunzi na walimu kuhusu ufundishaji wa insha kwa njia bora zaidi.
Isitoshe, kinamwandaa mwanafunzi kwa ajili ya mtihani wa insha, kinatoa changamoto za usomaji na namna ya kukabiliana na changamoto hizo. Ili kuboresha ufahamu wa mwanafunzi, mifano mwafaka imetolewa kwa kila insha. Hali kadhalika, kuna mazoezi ya kutathmini uelewa wa mwanafunzi chini ya kila kipengee. Tamrini maridhawa zimetolewa ili kumwandaa mwanafunzi katika insha za kiuamilifu pamoja na za kawaida.
Mitihani ambayo imetahiniwa kuanzia mwaka wa 2000 hadi 2015 imeshughulikiwa na majibu mwafaka kutolewa. Mitihani hii inamsaidia mwanafunzi katika kufahamu mbinu kadhaa zinazotumiwa katika utahini wa insha mbalimbali.
Mabadiliko hayana budi kuwepo katika maisha ya kila adinasi. Kutokana na haya, waandishi wa kitabu hiki wameangazia masuala ibuka, kwa mfano, utandawazi, ugatuzi, ugaidi pamoja na masuala mengineyo. Namna dunia inavyobadilika, ndivyo utunzi unavyozidi kuimarika. Insha zote zinazoshughulikiwa katika kitabu hiki zinafuata muundo ufaao, kwa hivyo mwanafunzi hatapata utata wowote katika kubainisha. Kwa hakika, mti hauendi ila kwa nyenzo.
Kitabu hiki kitakuwa cha manufaa kwa wanafunzi wa shule ya upili, vyuo vikuu pamoja na walimu na watafiti wa kipengee cha utunzi.
Reviews
There are no reviews yet.